2 Chronicles 6:12-42

Maombi Ya Solomoni Ya Kuweka Wakfu

(1 Wafalme 8:22-53)

12 aKisha Solomoni akasimama mbele ya madhabahu ya Bwana machoni pa kusanyiko lote la Israeli, naye akakunjua mikono yake. 13 bBasi Solomoni alikuwa ametengeneza jukwaa la shaba, urefu wake dhiraa tano, na upana wake dhiraa tano na kimo chake dhiraa tatu, naye akaliweka katikati ya ukumbi wa nje. Akapanda juu ya hilo jukwaa kisha akapiga magoti mbele ya kusanyiko lote la Israeli, akanyoosha mikono yake kwelekea mbinguni. 14 cAkasema:

“Ee Bwana, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe juu mbinguni wala chini duniani, wewe unayetunza Agano lako la upendo na watumishi wanaodumu katika njia yako kwa moyo wote.
15 dUmetimiza ahadi yako kwa mtumishi wako Daudi baba yangu, kwa kinywa chako uliahidi na kwa mkono wako umetimiza, kama ilivyo leo.

16 e“Sasa Bwana, Mungu wa Israeli, mtimizie mtumishi wako Daudi baba yangu ahadi zako ulizomwahidi uliposema, ‘Kamwe hutakosa kuwa na mtu atakayeketi mbele zangu kwenye kiti cha ufalme cha Israeli, kama wanao wakiangalia yote wayafanyayo kuenenda mbele zangu kama vile ulivyofanya.’ 17Sasa, Ee Bwana, Mungu wa Israeli, acha neno lako lile ulilomwahidi mtumishi wako Daudi baba yangu litimie.

18 f“Lakini kweli, je, Mungu atafanya makao duniani na wanadamu? Mbingu, hata mbingu zilizo juu sana, haziwezi kukutosha wewe. Sembuse Hekalu hili nililojenga! 19Hata hivyo sikiliza dua ya mtumishi wako na maombi yake kwa huruma, Ee Bwana Mungu wangu. Sikia kilio na dua ambayo mtumishi wako anaomba mbele zako siku hii ya leo. 20 gMacho yako na yafumbuke kuelekea Hekalu hili usiku na mchana, mahali hapa ambapo ulisema, ‘Jina langu litakuwako humo,’ ili kwamba upate kusikia maombi ambayo mtumishi wako ataomba kuelekea mahali hapa. 21 hUsikie maombi ya mtumishi wako na ya watu wako Israeli wakati wanapoomba kuelekea mahali hapa. Sikia kutoka mbinguni, mahali pa makao yako na usikiapo, samehe.

22 i“Mtu anapomkosea jirani yake na akatakiwa kuapa, akija na kuapa mbele ya madhabahu yako ndani ya Hekalu hili, 23 jbasi, sikia kutoka mbinguni na ukatende. Hukumu kati ya watumishi wako, ukimwadhibu yule mwenye hatia kwa kuleta juu ya kichwa chake yale aliyoyatenda. Umtangazie mwenye haki kwamba hana hatia, hivyo ukathibitishe kuwa haki kwake.

24 k“Wakati watu wako Israeli watakapokuwa wameshindwa na adui kwa sababu ya dhambi walizofanya dhidi yako, watakapokugeukia na kulikiri jina lako, wakiomba na kufanya dua kwako katika Hekalu hili, 25basi usikie kutoka mbinguni, ukasamehe dhambi ya watu wako Israeli na kuwarudisha katika nchi uliyowapa baba zao.

26 l“Wakati mbingu zitakapokuwa zimefungwa kusiwe na mvua kwa sababu watu wako wametenda dhambi dhidi yako, watakapoomba kuelekea mahali hapa na kulikiri jina lako nao wakageuka kutoka dhambi zao kwa sababu umewaadhibu, 27 mbasi usikie kutoka mbinguni na usamehe dhambi ya watumishi wako, watu wako Israeli. Wafundishe njia sahihi ya kuishi na ukanyeshe mvua juu ya nchi uliyowapa watu wako kuwa urithi.

28 n“Wakati njaa au tauni vikija juu ya nchi, au koga au kawa, nzige au panzi, au wakati adui atakapowazingira katika mji wao wowote, maafa ya namna yoyote au ugonjwa wowote unaoweza kuwajia, 29wakati dua au maombi yatakapofanywa na mmojawapo wa watu wako Israeli, kila mmoja akitambua taabu zake na uchungu wake, naye akainyoosha mikono yake kuelekea Hekalu hili, 30 obasi usikie kutoka mbinguni, katika makao yako. Usamehe na utende, umpe kila mtu kulingana na matendo yake, kwa kuwa unaujua moyo wake (kwa kuwa ni wewe peke yako ujuaye mioyo ya watu wote), 31 pili wakuogope kwa wakati wote watakaoishi katika nchi uliyowapa baba zetu.

32 q“Kwa habari ya mgeni ambaye si miongoni mwa watu wako Israeli, lakini amekuja kutoka nchi ya mbali kwa sababu ya jina lako kuu na mkono wako wenye nguvu ulionyooshwa, atakapokuja kuomba kuelekea Hekalu hili, 33 rbasi na usikie kutoka mbinguni, mahali pa makao yako, ukafanye lolote ambalo mgeni huyo anakuomba, ili mataifa yote ya dunia wapate kujua jina lako na wakuogope kama wafanyavyo watu wako Israeli nao wapate pia kujua kwamba nyumba hii niliyoijenga imeitwa kwa Jina lako.

34 s“Wakati watu wako watakapokwenda vitani dhidi ya adui zao, popote utakapowapeleka, wakati watakapoomba kwa Bwana kuelekea mji ambao umeuchagua, na Hekalu nililolijenga kwa ajili ya Jina lako, 35basi usikie dua na maombi yao kutoka mbinguni, ukawatetee haki yao.

36 t“Watakapotenda dhambi dhidi yako, kwa kuwa hakuna mtu yeyote ambaye hatendi dhambi, nawe ukachukizwa nao na kuwakabidhi kwa adui, ambaye atawachukua utumwani katika nchi iliyo mbali au karibu 37 una kama watabadilika mioyo yao katika nchi wanakoshikiliwa mateka, nao wakatubu na kukulilia katika nchi ya utumwa na kusema, ‘Tumetenda dhambi, tumefanya makosa na tumetenda uovu’; 38 vkama wakikugeukia kwa moyo wao wote na nafsi zao katika nchi ya adui zao ambao waliwachukua mateka, wakakuomba kuelekea nchi uliyowapa baba zao, kuelekea mji uliouchagua na Hekalu nililolijenga kwa ajili ya Jina lako, 39basi kutoka mbinguni, mahali pa makao yako, usikie dua yao na maombi yao na kuitetea haki yao. Uwasamehe watu wako, waliotenda dhambi dhidi yako.

40 w“Sasa, Mungu wangu, macho yako na yafumbuke na masikio yako yasikie maombi yaombwayo mahali hapa.

41 x“Sasa inuka, Ee Bwana Mungu,
na uje mahali pako pa kupumzikia,
wewe na Sanduku la nguvu zako.
Makuhani wako, Ee Bwana Mungu,
na wavikwe wokovu,
watakatifu wako na wafurahi
katika wema wako.
42 yEe Bwana Mungu, usimkatae
mpakwa mafuta wako.
Kumbuka upendo mkuu uliomwahidia
Daudi mtumishi wako.”
Copyright information for SwhNEN